Pages

Subscribe:

Ads 468x60px

Featured Posts

Tuesday, November 19, 2019

FAHAMU DALILI ZA KUSHUKA SUKARI MWILINI NA MATIBABU YAKE.

Kwa wagonjwa wa kisukari, tatizo la kushuka sana kwa sukari ni hatari zaidi kuliko tatizo la kupanda kwa sukari.
Kwa hali ya kawaida sukari ikishuka huweza kuua ghafla lakini sukari ya kupanda haiwezi kumuua mtu ghafla, hali hii iko zaidi kwa watoto wadogo na wagonjwa wa kisukari.
Sababu mbalimbali huweza kuchangia kushuka kwa sukari ghafla ikiwemo kuchoma dawa nyingi ya kushusha sukari, kuchelewa kula, kufanya mazoezi sana,kunywa pombe na saratani za kongosho.
Wakati sukari inashuka kuna dalili za mwanzo na dalili za mwishoni, kua makini sana na dalili za mwanzoni kwani kipindi hicho ndio unakua una uwezo wa kujiokoa lakini baada ya hapo unakua huwezi tena kujiokoa bila msaada kutoka kwa watu wengine.

dalili za mwanzo za sukari kushuka.

  • kizunguzungu
  • kutokwa jasho
  • njaa kali
  • wasiwasi
  • kichwa kuuma
  • kuloanisha mashuka kwa jasho wakati wa usiku
  • kuota ndoto za ajabu
dalili za mwisho baada ya sukari kushuka sana
  • degedege
  • misuli kuishiwa nguvu
  • kushindwa kuongea
  • kuchanganyikiwa
  • kupoteza fahamu
  • kuona ukungu.
vipimo
kwenye kipimo cha sukari au glucometer, pale inapokua chini ya 3.0mmol/l basi ni dalili kwamba sukari imeshuka sana na inaelekea kubaya.
    matibabu
    mgonjwa katika dalili za mwanzo anaweza kunywa glucose, juice au soda na kupata nafuu kisha kutafuta chakula na kukila, lakini mgonjwa wa dalili za mwisho anatakiwa akimbizwe hospitali kuwekewa sukari kwa njia ya mishipa au dripu.
    ni vizuri mgonjwa wa kisukari kuwaambia ndugu zake kuhusu dalili hizi ili waweze kumsaidia ikitokea hajiwezi kabisa.



    jinsi ya kuzuia hali hii.
    usichelewe kula; baada ya kuchoma dawa ya kushusha sukari au insulin basi hakikisha umekula kwa wakati ili kuzuia kuporomoka sana kwa kiwango cha sukari.
    pima kiwango cha sukari; kupima mara kwa mara ni njia pekee ya kujua kiwango chako cha sukari kikoje, sio kwa ajili ya kuogopa sukari inayoshuka tu ila hata ile ya kupanda ni hatari kwa afya yako kama ikiwa imepanda muda wote.
    kunywa pombe na chakula; sukari hushuka sana mgonjwa anapokunywa pombe bila chakula hivyo hakikisha umekula kwanza kabla ya kunywa pombe.
    mazoezi yako yaendane na dawa unayotumia; ukifanya mazoezi sana hakikisha unapunguza dozi ya dawa unayotumia kwani mazoezi hupunguza sana sukari mwilini.

                                                                                  STAY ALIVE
                                                           DR.KALEGAMYE HINYUYE MLONDO
                                                                    0653095635/0789846183

    FAHAMU DALILI ZA KUPANDA KWA SUKARI KWENYE DAMU NA MATIBABU YAKE.

    Kupambana na kiasi cha Sukari kwenye damu kwa wagonjwa wa kisukari ndio msingi mkuu wa matibabu ya ugonjwa wa kisukari kwani huepusha madhara makubwa yatokanayo na ugonjwa huu kama kuharibika kwa figo, ugonjwa wa presha, upofu. matatizo ya mishipa ya fahamu na kadhalika.
    Kwa kawaida sukari ya mgonjwa ikiwa zaidi ya 7.1mmol/l baada ya saa 8 bila kula au zaidi ya 10mmol/l saa 2 baada ya kula hutambulika kitaalamu kama hyperglaicemia au sukari ya juu kwa wagonjwa hawa.

    nini chanzo cha kupanda sukari kwa wagonjwa hawa?
    wagonjwa wengi wa sukari hupata tatizo la sukari zao kupanda sana hata kama wako kwenye dawa na hii husababishwa na sababu zifuatazo.
    kutomeza au kutochoma dawa kwa wakati: wagonjwa ambao hawamezi dawa au kuchoma sindano za sukari kama walivyoelekezwa na wataalamu wa afya huishia kupata tatizo la kupanda sukari juu kuliko kawaida.
    kula wanga mwingi sana; kimsingi wagonjwa wa sukari wanatakiwa wale vyakula vya wanga kidogo sana na siku zingine ikiwezekana wasile kabisa.
    Vyakula vya wanga kama ugali,wali, viazi, tambi, mihogo, chapati, mikate, maandazi, keki na kadhalika huongeza sukari sana ukilinganisha na vyakula vya protini na mafuta kama nyama, samaki, karanga, korosho, maziwa, mayai, na kadhalika.
    kuugua; mgonjwa wa sukari akiuugua ugonjwa wowote yaani kama malaria, typhoid, u.t.i au magonjwa yeyote mengine unayojua wewe lazima sukari ipande hivyo kwa kipindi hiki hata kama anapewa dawa za sukari, kama ugonjwa haujafahamika basi sukari haiwezi kushuka.
    msongo wa mawazo; msongo wa mawazo huchangia sana homoni zingine mwilini ambazo husababisha kupanda kwa sukari kwenye damu.
    kua mvivu; kama wewe ni mtu wa kufanya shughuli mbalimbali kama kutembea, kwenda kazini, kufanya kazi za nyumbani, kwenda mazoezini na kadhalika kisha ikatokea ukaacha hizo shughuli na kushinda nyumbani basi uko kwenye hatari ya kupandisha sukari mwilini.

    dalili za sukari kupanda ni zipi?
    • kusikia kiu sana
    • kichwa kuuma
    • kushindwa kutuliza akili sehemu moja.
    • kuona ukungu
    • kukojoa mara kwa mara 
    • kuishiwa nguvu
    • sukari kupanda zaidi ya 10mmo/l kwenye kipimo cha damu.
    hali hii ikiendelea kwa muda mrefu husababisha
    • magonjwa ya ngozi ya mara kwa mara
    • kuchelewa kupona kwa vidonda
    • ganzi
    • choo ngumu sana au kuharisha.

    matibabu ya hali yapi?
    matibabu ya sukari kupanda yanategemea sana chanzo cha ugonjwa husika cha kupanda kwa sukari hiyo na huweza kufanyika nyumbani au hospitali kama ifuatavyo.
    kunywa maji mengi; maji mengi husaidia sana kupunguza sukari mwilini kwa kuondoa sukari kupitia mkojo lakini pia huzuia kupungua kwa maji mwilini.
    fanya mazoezi; mazoezi husaidia sana kupunguza sukari, lakini ikiwa sukari imepanda usifanye mazoezi kwanza bila kuhakikisha kwamba umepima mkojo, ni hatari sana kufanya mazoezi iwapo mkojo wako una vitu vinaitwa ketones.
    badili mfumo wa chakula; epuka vyakula vya wanga na sukari na tumia muda mwingi kula vyakula vya ptotini na matunda ambayo hayana sukari.
    badilisha dawa; wakati mwingine dawa hazikufai au dozi ni kidogo hivyo onana na daktari wako anaweza kukubadilishia mfumo wa kumeza au akaongeza dozi.
    chukua vipimo; wakati mwingine ni ugonjwa mpya unakusumbua hivyo ni vizuri kwenda hospitali kupima magonjwa mbalimbali.

                                                                   STAY ALIVE

                                            DR.KALEGAMYE HINYUYE MLONDO
                                                          0653095635/0769846183

    JINSI UNAVYOWEZA KUISHI NA KISUKARI KWA MAZOEZI NA CHAKULA BILA DAWA.

    Ugonjwa wa kisukari ni moja ya magonjwa tishio ambayo yapo kwenye kikundi cha magonjwa ambayo sio ya kuambukizwa, ukitaka kujua zaidi kuhusu ugonjwa huu soma hapa....http://www.sirizaafyabora.info/2016/04/kabla-ya-ukoloni-utafiti-unaonyesha.html
                                                                 

    wagonjwa wengi sana pamoja na kutumia dawa mbalimbali bado hujikuta wanashindwa kuiweka sukari katika hali ya kawaida hivyo kujikuta wanakua na kiwango cha sukari juu muda wote.
    kiukweli hakuna mtu anayependa kumeza dawa au kuchoma sindano na ikitokea njia mbadala wa kuacha vitu hivyo kila mtu atafurahi kutumia njia hiyo.
    sasa katika matibabu ya kisukari wataalamu wengi na wagonjwa wengi husahua matibabu ya kwanza kabisa ambayo mgonjwa anatakiwa aanze nayo na ikishindikana ndio aanze dawa.

    matibabu ya kwanza ya kisukari ni yapi?
    kwa wagonjwa kisukari aina ya kwanza au type 1[ambayo hupata watoto wadogo mara nyingi] unatakiwa kuanza dawa hapo hapo kwani mgonjwa anakua hana insulin hata kidogo mwilini lakini kwa aina ya pili kitaalamu kama type 2 mgonjwa anatakiwa aanze mazoezi na diet kwanza kwani anakua anayo insulini mwilini lakini imeshindwa kufanya kazi vizuri sababu ya unene au insulin inazalishwa kidogo sana.
    watu wengi huanzishiwa dawa kwa kukosa nidhamu ya chakula na mazoezi lakini ukiwa na nidhamu hiyo huhitaji dawa kabisa.

    kwanini wagonjwa hawa wanaweza kutibiwa kwa mazoezi na chakula tu?
    sababu watu hawa tayari wana insulini mwilini ambayo haijaitoshelezi hivyo ukifanya mazoezi mwili husukuma sukari ndani ya misuli na kuipunguza kwenye damu na ukila vizuri kiwango cha sukari kitabaki kawaida na hautahitaji dawa kabisa.
    kimsingi mtu ambaye anahitaji nguvu za mwili kwa kutumia chakula cha wanga ndio ambaye sukari ni tatizo kwake lakini ukitumia njia tofauti kupata nguvu kama kwa kula vyakula vya protini na mafuta basi kisukari hakina ujanja.
     kiufupi ni kwamba kisukari ni ugonjwa wa watu ambao ni lazima wale wanga kama ugali, wali, viazi, mihogo, mikate, maandazi, chapati na kadhalika hivyo ukiamua kuachana na wanga basi umepona.

    mtu ambaye ameshatumia dawa miaka mingi anaweza kuacha dawa?
    ndio, kama ukiweza kufauata masharti ya chakula na mazoezi basi unaweza ukaacha dawa kabisa, kikubwa maisha hayo mapya yanatakiwa kua sehemu ya maisha yako sio kwamba ufanye hivyo kwa muda tu halafu uache.
    kimsingi watu wengi huugua kisukari na magonjwa mengine yasio ya kuambukizwa kwa kushindwa kula vizuri na kufanya mazoezi hivyo hata ambao hawaumwi wanatakiwa waishi kwa makini kwa kufanya mzoezi na kula vizuri.

    chakula gani cha kutumia kwa wagonjwa hawa ili waweze kuacha dawa?
    kwa mgonjwa ambaye tayari anatumia dawa au hatumii dawa diet ifuatayo kitaalamu kama ketogenic diet anatakiwa aanze nayo,  diet hii inalenga kuondoa kabisa vyakula vya wanga kwenye chakula chako na kuacha kiasi kidogo sana, ukitaka kujua zaidi kuhusu diet hii soma hapa......http://www.sirizaafyabora.info/2018/06/jinsi-unavyoweza-kupunguza-uzito-kwa.html

    mfano wa diet hiyo...

    asubuhi;
    yai mbili za kuchemshwa, kipande cha parachichi moja na chai ya rangi au maziwa isiyokua na sukari.

    mchana;
     samaki mmoja mkubwa au mdogo au dagaa  au robo kuku, mboga za majani nyingi, kipande cha parachichi moja na ndizi moja ya kupika au chapati.

    usiku; 
    samaki au  dagaa au robo kuku, mboga za majani za kutosha na kipande cha  parachichi.

    kumbuka kunywa maji mengi ya kutosha, baada ya kuanza diet hii kua makini na kiwango chako cha sukari  cha damu kwani utakiwa upunguze kiasi cha dozi ya dawa unazotumia au kuacha kabisa dawa ndani ya muda mfupi hivyo ukianza diet hii anza kupima sukari kila siku kuifuatilia.
    usile vayakula zaidi ya hivi nilivyotaja hapo juu ukiwa unaanza hata kama ni matunda usile kwani baadhi ya matunda ya sukari nyingi sana...unaweza ukapata hamu ya vyakula vingine kama binadamu lakini unaweza kujipangia kuvila siku maalumu kama kwenye sherehe au siku moja ya weekend kwa wiki kisha unarudi kwenye mfumo wako.
    kama kiwango chako cha lehemu au cholestrol kiko vizuri unaweza kula na nyama ya ngombe, mbuzi au nguruwe.
    kumbuka, pamoja na faida za  kuacha dawa, diet hii itakupunguza sana uzito kitu ambacho ni muhimu sana kwa wagonjwa wa kisukari.

    mazoezi gani unaweza kufanya?
    nunua kamba kaa nayo nyumbani kwani watu wengu hukosa muda wa kwenda gym kisha fanya mazoezi ya kuruka kamba angalau kuruka mara 500 kila jioni au asubuhi.
    unaweza ukafanya haya mazoezi angalau mara tatu au nne kwa wiki.
    kama una nafasi ya kufanya mazoezi ya aina ya aina nyingine pia unaweza kufanya, kama kazi zako ni ngumu za kutoa jasho  au unatumia baiskeli kwenye shughuli zako basi hauhitaji tena mazoezi.

    mifano hai;
    kuna watu wengi mabao wameacha dawa kwa kufauta masharti haya, mwezi uliopita kaka yangu mmoja alinipigia simu,  sukari ikiwa imemuanza kwa mara ya kwanza maishani mwake akiwa na sukari ya 26mmol/l na alikua ameshapewa dawa za kuanza.
    nikamwambia aanze diet hii, na baada ya siku tatu sukari tu  yake ilikua 4.6mmol/l ambayo ni kawaida kabisa.
    lakini pia ukiingia mtandaoni utakutana na watu wengi sana walio acha dawa kwa kutumia hii ketogenic diet.


                                                                                STAY ALIVE

                                                  DR.KALEGAMYE HINYUYE MLONDO
                                                                 0653095635/0769846183
                                                                  

    UFAHAMU UGONJWA WA KISUKARI NA MATIBABU YAKE.

    kabla ya ukoloni utafiti unaonyesha palikua hakuna wagonjwa wa kisukari kwa nchi za kiafrika lakini miaka mingi baada ya ukoloni na kutawaliwa na kupata uhuru wagonjwa waafrika wa kisukari walianza kuonekana. hii ni kwasababu ya mabadiliko ya ulaji wa vyakula na kuingia kwa tamaduni za kizungu ambazo ni tofauti na za kwetu ambzo tamaduni hizi huchangia kwa namna moja au nyungine kuleta ugonjwa huu mfano kutumia gari muda mwingi bila mazoezi, kushinda ofisini umekaa, kuangalia tv na kadhalika.

    ugonjwa wa kisukari ni nini?
    huu ni ugonjwa ambao huanza kujionyesha kwa kua na sukari nyingi kwenye damu sababu ya kongosho kushindwa kabisa kutengeneza homoni ya insulini au kutengeneza insulini kidogo sana ambayo insulini hii huhusika moja kwa moja kushusha sukari mwilini.
    hali hii huleta madhara mbalimbali kwenye viungo vya binadamu na isipo shughulikiwa huweza kuleta kifo cha mapema kabisa.

    kuna aina mbili za kisukari
    type 1 diabetes; aina ya kisukari ambayo husababishwa na kongosho kushindwa kabisa kutoa insulin mara nyingi hutokea pale ugonjwa fulani unaposhambulia kongosho hilo. hutokea mara nyingi kwa watoto na ni aina ya sukari ambayo huua kirahisi sana.

    type 2 diabetes; hii ni aina ya kisukari ambayo hutokea mara nyingi kwa watu wazima zaidi ya miaka 45 na kongosho hapa hutoa insulini kidogo ambayo haitoshi kupunguza sukari mwilini.

            watu wenye hatari ya kuugua kisukari

    • familia au ukoo wenye historia ya kisukari
    • unene na vitambi
    • umri zaidi ya miaka 45
    • historia ya kuugua kisukari cha mimba
    • presha kubwa ya damu
    • lehemu nyingi kwenye damu[cholestrol
    • matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi.
    • ulevi wa kupindukia na uvutaji wa sigara.
    • kutofanya mazoezi kabisa.
    • ulaji mkubwa wa nyama hasa nyama nyekundu.


    dalili za ugonjwa wa kisukari

    • kukojoa mara kwa mara
    • kupata kiu kikali cha maji mara kwa mara
    • kusikia njaa sana mara kwa mara
    • kupungua uzito hata kama ulikua mnene.
    • kuchelewa kupona kwa vidonda vya kawaida
    • kutoona vizuri
    • kuchoka sana
    • kukojoa mkojo wenye sukari
    • kutoona vizuri


    vipimo ambavyo hufanyika
    mgonjwa hupimwa damu asubuhi akiwa bado hajala chochote na kama sukari ikionekana ni zaidi ya 7.0g/dl basi ana kisukari au kama akipimwa masaa kadhaa baada ya kula na sukari ikazidi 11g/dl basi huyo ni mgonjwa wa sukari.

    matibabu
    hapa ndipo watu wengi wamepoteza pesa zao kwa waganga wa kienyeji...ugonjwa huu ukishaanza hauponi hata iweje, kinachofanyika ni kwamba utapewa huduma itakayo kufanya kuondoa dalili za sukari, kuepusha madhara ya sukari kua juu mwilini na wewe kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine.

    matibabu ya type 1 diabetes; mgonjwa huyu hana insulini hata kidogo mwilini hivyo atachomwa sindano ya insulin asubuhi na jioni kwa maisha yake yote bila kuacha. ni ngumu kidogo mwanzoni kujichoma mwenyewe lakini baada ya muda fulani unazoea.kumbuka mgonjwa huyu hatumii vidonge  vya kupunguza sukari kabisa.

    matibabu ya type 2 diabetes;matibabu ya kwanza kabisa ya mgonjwa huyu ni mazoezi na chakula bora na akifanikisha hili anaweza asitumie dawa kabisa lakini sababu watu wengi hawana nidhamu ya chakula na mazoezi basi watu hawa huanzishiwa vidonge ambavyo husaidi mwili kutengeneza sukari zaidi ili kuipa nguvu ile kidogo inayotengenezwa. wakati mwingine baada ya muda mrefu wagonjwa hawa sukari yao ikishindwa kudhibitiwa na vidonge huhamia kwenye sindano. mfano wa dawa zilizopo ni metformin,gibenclamide, tolazamide na etc

    madhara ya ugonjwa wa kisukari
    kufa kwa figo; figo inapochuja damu yenye sukari nyingi huchoka mapema na baadae hushindwa kabisa kufanya kazi.

    kufa kwa mishipa ya fahamu; sukari nyingi kwenye damu huharibu mishipa ya fahamu na baadae mgonjwa huanza kupata ganzi sana hasa miguuni na huweza kukanyaga vitu vyenye ncha kali bila kusikia maumivu.

    upofu; eneo maalumu kwa ajili ya kumfanya binadamu aone kitaalamu kama retina huharibiwa kwa uwepo wa sukari nyingi kwenye damu.

    kidonda cha mguu; kitaalamu huitwa diabetic foot, kidonda hichi huanza chenyewe bila maumivu yeyote na mtu anaweza asikione kama kipo chini ya nyayo. hiki ndio chanzo kikuu cha wagonjwa hawa kukatwa miguu kwani kidonda kinaweza kikapanda mpaka juu bila kuonekana.

    kiharusi; huu hutokea pale mishiba ya damu inapozibwa kichwani kwa kiasi kikubwa cha mafuta na cholestrol ambavyo vyote huambatana na ugonjwa huu pia.

    presha ya damu; ugonjwa huu huongeza uzito[viscosity] wa damu na kuweka vikwazo kwenye mishipa ya damu na kusababisha moyo kutumia nguvu nyingi kusukuma damu na kusababisha presha.

    kuishiwa nguvu za kiume; nguvu za kiume zinategemea sana msukumo wa damu kukaa kwenye uume ili kuleta ule ugumu sasa kwenye kisukari hutokea mafuta na cholestrol ambavyo huziba ile mishipa midogoya damu ya kwenye uumenna kusababisha nguvu hizo kuisha kabisa na uume kua mdogo.hili ni tatizo kubwa kwa wagonjwa hawa.
    madhara mengine ni kubadilika kwa ngozi na kua nyeusi, magonjwa ya mishipa ya damu na kuharibika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.

                                     elimu kwa mgonjwa wa kisukari
    • wagonjwa wengi sana wamekufa kwa kutozingatia masharti na kujifanya wao wanawajua vizuri waganga wa kienyeji. wengine waliacha dawa baada ya kupata vikombe vya babu na kufa baada ya muda. kama wewe unaamini waganga wa kienyeji wana dawa basi hakikisha sukari yako inapimwa kila siku kuona kama kweli inashuka kipindi unatumia dawa hizo. ugonjwa huu hauponi na kama uko kwenye dozi ya kuuponya basi ujue unapoteza muda na pesa zako.
    • hakikisha unafanya mazoezi angalau nusu saa kwa siku hata ya kutembea tu kwani husaidia sana kuchoma mafuta na kutengeneza insulini mwilini hasa kwa wagonjwa wa type 2
    • nunua mashine ya kupima sukari ya kwako mwenyewe kwani ugonjwa huo ni wako, mwili huo ni wako na ukifa utazikwa peke yako wala sio na daktari au mtu yeyote anayekuuguza hivyo usisubiri kufuatiliwa.hivyo hakikisha unapima sukari yako hata mara nne kwa wiki kujua kama iko sawa na kama ndio mgonjwa mpya pima kila siku kwanza mpaka utakapoona sukari imetulia.
    • kula vizuri;hapa ndio mzizi mkuu wa huu ugonjwa..ukileta uzembe hapa unakufa na nina fahamu watu walioambiwa wakasema kuliko nisile kitu fulani bora nife na walikufa kweli..kula vizuri...narudia kula vizuri.... uepuke vyakula vyenye sukari na wanga mwingi kama soda,biskuti, chocolate na  kadhalika.utafiti mpya unaruhusu mgonjwa huyu kula vyakula karibia aina zote ila kwa kiasi kidogo mfano wali kidogo, ndizi kidogo, viazi mviringo kidogo,ugali kidogo, samaki kwa wingi, mboga za majani kwa wingi, matunda ambayo hayana sukari nyingi kwa wingi.
    • ulevi wa kupindukia; unywaji mkubwa wa pombe huua kongosho japokua unywaji  kawaida ni mzuri kwa moyo hivyo epuka ulevi wa kupinduki kwani utakumaliza mapema.
    • hudhuria clinic ya kisukari; huku utajifunza mambo mapya kuhusu kisukari lakini pia daktari anaweza kugundua shida yako mpya ambayo wewe hujaiona na  pia clinic hizi zitakukutanisha na walioishi na kisukari miaka mingi bila kusumbuliwa nacho.
    • mwisho; idadi ya wagonjwa wa kisukari imeongezeka kutoka wato milion 108 mwaka 1980 mpaka watu milion 422 mwaka 2014. mwaka 2016 utafiti mpya unaonyesha katika kila watu 11 mmoja ana kisukari. zaidi ya watu milioni moja na nusu hufa kila mwaka sababu ya ugonjwa huu lakini pia ndio ugonjwa unaoongoza kusababisha upofu, kukatwa miguu,kiharusi, shinikizo la moyo na kuua figo.                                   
                                                            STAY ALIVE       
                                   DR.KALEGAMYE HINYUYE MLONDO
                                                       0653095635/0769846183

                                   
                                               
     
    Blogger Templates